Video sanaa ni aina nyingine ya filamu yenye kuonesha matukio halisi kwa mtazamo wa kisanaa, Pia huhusisha matumizi ya vinyago, michoro, uhariri picha na mifumo mingine ya sanaa katika kuwasilisha ujumbe wake. Lois Patiño ni msanii tokea nchini Hispania aliyefika hapa Tanzania kwa mwaliko toka ubalozi wa uhispania Embassy of Spain in Dar es Salaam ili kuendesha warsha ya video sanaa kwa vijana wakitanzania pale Nafasi Art Space. Kazi za Lois ni za kipekee mno na ameweza kuzionesha nchi mbalimbali ikiwemo Marekani, Uingereza, Indonesia na hata Tanzania. Kazi yake maarufu zaidi ni Pwani ya Mauti (Coast of Death) ambayo imemletea tuzo nyingi sana na heshima kubwa katika ulimwengu wa video sanaa. Hii ni Tafsiri ya mahojiano mafupi yaliyofanika kati ya Lois Patiño na Habib Dil walipokutana.
Habib: Sinema ni Mauti kazini (Cinema is death at work) ndio kauli mbiu iliyotawala katika mitandao yako ya kijamii. Kwa nini Mauti?
Lois: Watu wengi huniuliza hivyo, msichokijua ni kuwa huo si msemo wangu bali ni msemo wa mtengeneza filamu mwingine aliyenivutia kuingia katika sanaa. Na yeye husema hivyo kwa maana kuwa filamu ni kunasa picha jongezi za nyakati fulani. Wakati ukipita basi umepita, hiyvo wakati huo ndio umekufa. Hivyo filamu ni Mauti kazini.
Habib:Umesomea saikolojia ya akili ya mwanadamu katika chuo kikubwa nchini Hispania, kwa nini ukaamua kuukacha uanasaikolojia na kujikita kwenye filamu.
Lois: Nilikuwa na mapenzi ya filamu tangu nikiwa kijana mdogo. Nilipenda kusomea saikolojia ili tu kujua ni jinsi gani akili ya mtu hutenda kazi, namna ambavyo binadamu hutofautiana kifikra, mtazamo hadi muonekano. Chukulia mfano, kuna mwanamke anayetembea bila nguo mbele yetu, kuna watu watasema ni kichaa, wengine watasema ni kazi ya sanaa, wengine wataghafirika, wengine watampa nguo avae na wengine watafurahia na wapo watakao mtamani. Huu utofauti wa kifikraa ndio hasa nilikuwa nikiusaka na uelewa nilioupata ndio ninaoutumia kuunda filamu zangu. Naweza kusema nilisomea saikolojia kwa ajili ya kujijenga ila filamu ilikuwa tayari ikiishi ndani yangu.
Habib: Katika warsha uliweza kudadavua video sanaa katika mifumo tofauti, ni vipi unaweza kuirahisisha kwa uelewa zaidi.
Lois: Kwa urahisi, ninaweza kusema video sanaa zimegawanyika katika mifumo mitatu ambayo ni Video art, Video installation na experimental video. Video art hutumia matukio halisi na huwa na kisa au simulizi ama ujumbe msanii anataka kuuwasilisha. Uzuri wa kazii hii huwa katika upigaji na uhariri picha lakini pia ujumbe wenyewe. Mfumo wa pili ni Video installation, hii huhitaji akili ya ziada, idadi kubwa ya watu na technologia kwani huhusisha zaidi matumizi ya mwanga, miale na viuli katika kuwasilisha jambo. Pia jkatika mfumo huu ndio sanaa nyingine kama uchoraji, uchongaji n.k huhusika zaidi. Mfumo wa tatu ni Experimental video. Hii ni tofauti kiasi na zingine, hapa muundaji huwa na wazo ambalo anapaswa kulifanyia majaribio, sasa yeye hunasa shughuli nzima katika picha hadi pale anapofikia jawabu lake. Mfano ninataka kujua jinsi gani maji yamoto yanaganda katika hewa wazi ya baridi. Basi nitatega camera zangu msimu wa baridi nakuchukua picha kuanzia mwanzo ninavyochemsha maji hadi ninapoyamwaga hewani na kubadilika kuwa barafu. Hapo nimefanya uchunguz na kuuhifadhi katika video, ndio maan inaitwa experimental.
Habib: Wakati ninatazama baadhi ya kazi zako nimegundua kuwa unatumia picha zilizopigwa kwa urefu (Long shots). Kuna sababu gani kutumia mtindo huu kwa wingi?
Lois: Ninapenda sana mazingira, hivyo ninategesha kamera yangu mbali na kitu ninachopiga picha ili kuonesha uhusiano uliopo baina ya kitu na mazingira yaliyokizunguka. Pia huwa ninachukua matukio halisi ya kimaisha, hivyo kuwa mbali na kitu ninachokipiga picha huleta uhalisia. Mfano, ninapowapiga picha watu wawili walio ufukweni nikiwa mbali, basi wataendelea na shughuli zao kama kawaida, ila nikiwa karibu ninaweza kuwaudhi kwa urahisi au kuwatia hofu na kupelekea kuondoa uhalisia wa matendo yao katika picha, Hivyo kwangu umbali ni muhimu sana.
Habib: Aina ya filamu unayofanya huenda ni kitu kigeni hasa barani Africa kwani kwa kutazama ufupi wake, ukosefu wa hadithi, matumizi ya michoro, vinyago na kadhalika. Huwa unaonesha wapi kazi za aina hii?
Lois: Aina hii ya filamu huwa ni kwa ajili ya majumba ya sanaa, japo zipo chache ambazo hupelekwa kwenye majumba ya sinema. Mimi binafsi hupenda kuonesha kazi zangu kupitia vitambaa au miili ya watu ambao wanahudhuria maonesho yangu, ninaakisi cinema yangu kwenye nguo walizovaa tu. Huo ni mtindo wangu hivyo siwezi upeleka sinema. Na aina hii ya filamu ilianza mapema hasa mwanzo tu wa vita ya kwanza ya dunia. Nadhani ni aina nzuri kwa mtu yoyote kufanya ikiwa anahisi hana mtaji wa kufanya filamu za kawaida. Aina hii ya filamu ni muhimu katika kujijenga, kijitangaza na hupanua fikra.
Habib: Unadhani aina hii ya filamu inaweza kumuingizia mtu kipato cha kukidhi mahitaji yake yote.
Lois: Sio tu aina hii ya filamu, ni kazi yoyote ya sanaa inaweza kumuingizia mtu kipato na kumpeleka katika ardhi ambazo hakuwahi tegemea. Kinachohitajika hasa ni juhudi, ueledi, uthubutu na upekee. Mimi nina namna yangu inayonitofautisha na watengeneza video sanaa wengine, hapa Tanzania kuna hadithi nyingi, mazingira mazuri, watu wengi na utamaduni uliojitosheleza. Nadhani vijana wakitumia hii fursa na kujua hazina iliyopo nyumbani kwao basi wataweza kutajirika. Kosa kubwa wanaloweza kulifanya ni kutuiga sisi wa ulaya. Utajiri wa sanaa upo katika mila, tamaduni, desturi na lugha. Wakishikilia hapo kwa kweli watakidhi mahitaji yao japo siwezi kuwahakikishia kuwa watafanikiwa katika mahitaji yao yote.
Warsha hiyo ilihusisha mafunzo ya nadharia na vitendo lakini pia kuangalia kazi zingine na kujadiliana. Wanafunzi wote walipaswa kuandaa kazi baada ya mafunzo. Jumamosi ya tarehe 25 mwezi wa 8 2018 onesho lilifanyika Nafasi Art Space, Lois Patiño aliweza kuonesha kazi zake na pia wanafunzi wa warsha hiyo walionesha kazi walizofanya baada ya kuhitimu mafunzo na kutunukiwa vyeti.
Nafasi Art Space inatoashukrani kwa Habib Dil na Tuongee sanaa kwa kuruhusu sehemu ya mahojiano yake kutumika katika ukurasa huu. Unaweza kutembelea mtandao ufuatao ilikutazama kazi mbalimbali za Lois Patiño https://vimeo.com/loispatino